Jumapili 15 Februari 2026 - 18:30
Uhusiano wetu na Iran ni wa kihistoria, wa kina na wenye mizizi imara

Hawza/ Harakati ya Amal nchini Lebanon imeandaa hafla ya kumheshimu Mojtaba Amani, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, harakati ya Amal inayoongozwa na Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon, iliandaa hafla hiyo kwa heshima ya Mojtaba Amani kutokana na huduma na shughuli zake. Katika tukio hilo, Khalil Hamdan, mwakilishi wa Spika wa Bunge, alihudhuria.

Katika hafla hiyo pia walihudhuria watu mashuhuri, miongoni mwao Sheikh Ali Al-Khatib, Naibu Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia wa Lebanon; Hamid Al-Khaffaf, mwakilishi wa Ayatollah Ali al-Sistani; Ahmad Sweidan, balozi wa Lebanon nchini Iran; Tawfiq Samadi, naibu balozi wa Iran; pamoja na wabunge kadhaa na ujumbe wa Hezbollah ulioongozwa na Ammar al-Mousawi, mkuu wa mahusiano ya kimataifa wa chama hicho.

Aidha, viongozi na wanachama wengine wa Amal, washauri wa ubalozi wa Iran, wawakilishi wa taasisi za kidini na kielimu, pamoja na vyombo vya habari vya ndani na vya kimataifa walishiriki.

Sherehe ilianza kwa kusomwa aya za Qur’ani Tukufu na msomaji Luqman Ayyash, kisha ukapigwa wimbo wa taifa wa Lebanon, wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wimbo wa harakati ya Amal. Uendeshaji wa hafla ulisimamiwa na Mohammad Jaradi.

Baadaye, Khalil Hamdan alianza hotuba yake kwa kusema: “Ni heshima kuhudhuria kwa niaba ya ndugu yangu mheshimiwa Spika wa Bunge Nabih Berri katika hafla ya kumheshimu balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bw. Mojtaba Amani. Niruhusuni nifikishe salamu na pongezi za Spika wa Bunge na ndugu zangu katika harakati ya Amal kwenu, na kupitia kwenu kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ali Khamenei, pamoja na uongozi na wananchi wa Iran. Tuko katika siku za kumbukumbu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na Ruhollah Khomeini, na ahadi yetu ni ile ile ya Musa al-Sadr — Imamu ambaye athari na fikra zake bado zinasikika.”

Aliongeza kuwa; mwanzo wa njia hii ulikuwa wakati Imam Musa al-Sadr alipofika Lebanon na kuzungumza katika mji wa Tyre kuhusu fikra na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na kufichua uhalifu wa utawala wa Pahlavi. Alisema harakati ya Amal — kuanzia Imam Musa al-Sadr hadi Mostafa Chamran, kutoka Nabih Berri hadi mashahidi wa njia ya mapambano — bado imeshikamana na ahadi hiyo.
“Uhusiano wetu na Iran ni wa kihistoria, wa kina na wenye mizizi imara; kuanzia wanazuoni wa zamani hizo hadi leo, kuna uhusiano usiovunjika kati ya Lebanon na Iran,” alisisitiza.

Hamdan alibainisha kuwa; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa msimamo wake thabiti katika nyanja mbalimbali, ni mfano wa uhuru wa kielimu na ustahimilivu, na taifa linalolipa gharama ya kuwatetea waliodhulumiwa wakati wengine wanachochea migawanyiko ya kidini na kimadhehebu.

Akizungumza na balozi wa Iran, alisema: “Ulishiriki huzuni za Lebanon kabla ya kushiriki furaha zake, na hata ulipojeruhiwa katika tukio la mlipuko wa ‘Bejer’, hukuacha kuitumikia Lebanon. Adui Mzayuni hakufanikiwa kukuzuia kutekeleza wajibu wako. Wewe ni mtoto wa Mapinduzi na wa familia iliyotoa mashahidi kwa ajili ya ushindi na kuendelea kwa Mapinduzi. Leo badala ya kukuaga, tunasema hadi tuonane tena katika jukumu lako jipya nchini Iran, tukikutakia mafanikio na afya njema.”

Mjumbe huyo wa Amal alirejelea pia matukio ya karibuni, alisema:
“Jana katika kijiji cha Yanooh tulishuhudia kuuawa kwa mtoto Ali Hassan Jaber, baba yake shahidi Hassan Jaber kutoka vikosi vya usalama wa ndani, na shahidi Ahmad Ali Salameh. Wakati huo huo huko Aita al-Shaab kulikuwa na shahidi mwingine na majeruhi kadhaa kutokana na uvamizi wa Israel, na katika eneo la Arqoub raia mmoja alitekwa nyara katika njia ya kutatanisha huku kamati ya ‘Mechanism’ ikiwa kimya. Hii ndiyo simulizi ya ustahimilivu wa kusini mwa Lebanon; mahali ambapo mtoto huzaliwa alfajiri na jioni anakuwa shahidi.”

Aliuliza: “Je, Imam Musa al-Sadr aliona mbele aliposema: Adui hutuweka kati ya chaguo mbili — kuwa mashahidi au kuwa wahanga?”

Baadaye, balozi wa Iran Mojtaba Amani alitoa hotuba akimshukuru Nabih Berri na uongozi wa harakati ya Amal kwa kuandaa hafla hiyo.
Alisema: Uhusiano kati ya Lebanon na Iran ulianza tangu siku za mwanzo za Mapinduzi ya Kiislamu, wakati Mostafa Chamran — aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Iran — alipofika Lebanon. Sasa miaka 47 imepita tangu ushindi wa Mapinduzi, na katika kipindi hicho Iran imekabiliwa na njama nyingi kama mauaji ya kisiasa, majaribio ya mapinduzi ya kijeshi na matumizi ya teknolojia na maadui dhidi yake, lakini juhudi hizo zote zimeshindwa kutokana na azma ya wananchi wa Iran.

Amani alisisitiza: “Tunakabiliana na changamoto ima kupitia vita, mazungumzo au ustahimilivu, kama ambavyo watu wa Lebanon wanavyokabiliana na uvamizi kwa ustahimilivu na mapambano. Uzoefu wangu nchini Lebanon umekuwa mzuri sana, na licha ya jeraha la tukio la Bejer na kuuawa kwa wapendwa kama Hassan Nasrullah, kukabiliana na Israel ni wajibu mtakatifu. Tunajiona kuwa wafuasi wa haki na tutadumisha uhusiano kati ya mataifa haya mawili.”

Mwisho wa hafla, Khalil Hamdan alimkabidhi balozi wa Iran zawadi ya kumbukumbu iliyopewa jina “Mshirika wa Majeraha na Ustahimilivu.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha